Mke wa Raisi wa China ateuliwa kama mwakilishi maalum wa UNESCO

27 Machi 2014

 

Peng Liyuan, ambaye ni mwanamuziki maarufu na pia mke wa raisi wa China, ameteuliwa kama mwakilishi maalum wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, kuhusu mwendeleo wa elimu kwa wanawake na watoto wa kike.

Akizungumza wakati wa kumteua Peng Liyuan huko Paris, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, amesema kwamba elimu kwa wanawake na watoto wa kike ni haki ya msingi, na njia bora ya kuimarisha maendeleo. Ameongeza kwamba, ili kufanikiwa katika malengo ya maendeleo, tunahitaji mifano kama ya Peng Liyuan, ambaye ni mfano kwa wasichana wote China na pia duniani.

Peng Liyuan amechaguliwa kutokana na juhudi zake katika kuwezesha wanawake, kuimarisha elimu, usawa wa kijinsia, ambayo ni malengo ya shirika la UNESCO.

Mwalimu wa kwanza wa mtoto ni mama yake, amesema Peng Liyuan wakati akipokea uteuzi, huku akisisitiza majukumu ya kina mama katika kutokomeza umaskini na kuleta maendeleo endelevu kwa wote.

Uteuzi huu umetokea wakati ambapo rais wa China amekuwa ni kiongozi wa kwanza wa China kutembelea shirika la UNESCO. Mkurugenzi mkuu wa UNESCO Bi Bokova amipongeza China kwa hatua iliyochukua kuwekeza pesa katika sekta za elimu, sayansi na utamaduni, hatua zinazochangia pakubwa katika maendeleo yake ya kiuchumi na kijamii.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud