Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa walaani shambulio hotelini mjini Kabul

Umoja wa Mataifa walaani shambulio hotelini mjini Kabul

Ofisi ya Umoja wa Mataifa Afghanistan UNAMA imeshutumu vikali shambulio la jana usiku lililotokeaSerena Hotel, mjini Kabul, ambapo watu tisa waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Shambulio hilo, linalodaiwa kuhusishwa na Taliban, limetekelezwa siku moja kabla ya maadhimisho ya tamasha la Nowruz, ambapo, kwa mujibu wa UNAMA, ni wakati wa kuweka amani na mshikamano katika jamii.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo, Ján Kubiš, amesema kwamba wataliban wanapaswa kuheshimu utaratibu wa kipindi cha mpito akiongeza kwamba anaudhika na azimio lao la kutaka kushambulia mchakato wa uchaguzi kwa nguvu na tishio.

Shambulio la jana linafuata lingine na kujilipua siku tatu zilizopita katika mkoa wa kaskazini, likiua wananchi 15 na kujeruhi takriban watu wengine 50.

Mashumbulizi hayo yanatokea wakati wa maandalizi ya uchaguzi wa rais na mabaraza ya mikoa unaotarajia kufanyika tarehe 5, mwezi Aprili.