Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya ICJ itathmini uwepo wa Israel kwenye maeneo ya Palestine: Richard Falk

Mahakama ya ICJ itathmini uwepo wa Israel kwenye maeneo ya Palestine: Richard Falk

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu maeneo ya Wapalestina yalokaliwa, Richard Falk, ametoa wito kwa mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, itathmini hali ya Israel kuendelea kuwepo kwenye maeneo ya Palestina, na madai kuwa hali hiyo ina sifa za ukoloni, ubaguzi wa rangi na uangamizaji ya kimbari.

Amesema hatua maalum zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu za watu wa Palestina zimelindwa, na utawala wa sheria kuwekwa katika hali hiyo ambayo imedumu zaidi ya miaka 45.

Bwana Falk amesema hayo katika ripoti yake ya mwisho katika wadhfa wake, baada ya kuhudumu miaka 6 kama mtaalam huru aliyeteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu kufuatilia na kuripoti kuhusu hali ya haki za binadamu katika maeneo ya Palestina yalokaliwa tangu mwaka 1967. Ametoa wito pia kwa Baraza la Haki za Binadamu kutathmini hali hiyo kisheria, na kuiomba jamii ya kimataifa kulishughulikia suala la haki za binadamu za WaPalestina kwa njia mathubuti na yakinifu.