Urusi yatumia kura turufu kupinga azimio dhidi ya kura ya maoni Crimea

16 Machi 2014

Rasimu ya azimio la Baraza la Usalama iliyokuwa na lengo la kupinga kura ya maoni inayofanyika kwenye jimbo linalojitawala la Crimea huko Ukraine imegonga mwamba baada ya Urusi kutumia kura yake turufu kuipinga huku China ikiepuka kuonyesha upande wowote ilihali wajumbe 13 waliunga mkono.

Kwa mujibu wa kanuni za baraza la usalama kura turufu ina uwezo wa kuzuia kupita kwa azimio lolote la baraza hata kama wajumbe wengi wataunga mkono. Baraza hilo lina wajumbe watano wenye kura turufu ambao ni China, Ufaransa, Uingereza, Urusi na Marekani.

Kura ya maoni Crimea inafanyika tarehe 16 mwezi huu kuamua iwapo jimbo hilo lijitenge na Ukraine na kujiunga na Urusi ambapo rasimu hiyo ilikuwa inasema inazingatia umoja, utaifa na mamlaka ya Ukraine.

Wakizungumza baada ya azimio hilo kupingwa kwa kura turufu, mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power amesema Urusi inaweza kuwa na uwezo wa kutumia kura turufu kupinga azimio hilo lakini haiwezi kupinga kile alichosema ni ukweli.

Hata hivyo mwakilishi wa kudumu wa Urusi Balozi Vitaly Churkin amesema hatua ya nchi yake inazingatia msingi wa rasimu hiyo ya kwamba kura ya maoni ni kinyume cha sheria na kwamba serikali yake itaheshimu uamuzi wa Crimea.