Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mifumo ya sheria ya kitaifa yafaa iwajali watoto: OHCHR

Mifumo ya sheria ya kitaifa yafaa iwajali watoto: OHCHR

Watoto wengi duniani hawapati haki kwa maovu na uhalifu unaotendwa dhidi yao kwa sababu wanaogopa kudhulumiwa, kunyanyapaliwa na kutelekezwa au kuadhibiwa wao na familia zao, imesema ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, OHCHR.

Ofisi hiyo imesema upatikanaji wa haki ni mgumu hasa kwa watoto wanaoishi katika nyumba za malezi, watoto wahamiaji, wale wanaoishi katika umaskini ulokithiri au wale wanaokabiliwa na kudhulumiwa na watu walioko katika mazingira wanamoishi.

Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Flavia Pansieri amesema kuwa serikali zinapaswa kuweka mifumo ya sheria inayowajali na kuwawezesha watoto kudai haki zao.

Akilihutubia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wakati wa kuanza mjadala wao wa kila mwaka kuhusu haki za mtoto, Bi Pansieri amesema mifumo ya sheria ya kitaifa inatakiwa iwe na uwezo wa kupokea na kushughulikia malalamishi ya watoto, au kwa niaba yao.

 

 

“Ili wawezeshwe vyema, watoto wanatakiwa kuelewa kabla kukubali maamuzi yanayowahusu, kulingana na uwezo wao mdogo. Wanapaswa kufahamu na kupata maelezo kuhusu haki zao na jinsi ya kusaidiwa. Watoto wanapaswa wawe na uwezo wa kuanzisha mashtaka pale Ambato haki zao zimekiukwa. Maoni ya watoto, hata ya wale wadogo mno, yanatakiwa kuzingatiwa vyema. Watoto pia ni lazima walindwe kutokana na kudanganywa, kudhulumiwa, kuadhibiwa na mateso, na wataalam wote husika ni lazima wawe na ujuzi na stadi zinazohusiana vyema na haki za watoto”

Bi Pansieri amesema mfumo wa sheria unaowajali watoto ni ule unaoelewa na kuheshimu haki za watoto na hatari wanazokabiliwa nazo, wakija kama waathiriwa, mashahidi au walalamishi, na wakati mwingine, sababu za malezi au ulinzi.