Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apongeza makubaliano ya kukutanisha familia kwenye rasi ya Korea.

Ban apongeza makubaliano ya kukutanisha familia kwenye rasi ya Korea.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amekaribisha makubaliano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK na Jamhuri ya kufanya ukutanishaji wa jamaa kwenye Mlima wa Kumgang kati ya Februari 20-25 kama ilivyopangwa.

Taarifa ilotolewa na msemaji wake inasema kuwa Katibu Mkuu ametiwa moyo hasa na makubaliano hayo baada ya wito alioutoa kwa rais wa bunge la DPRK, Kim Yong Nam wakati alipokuwa Sochi kwamba aonyeshe kulegeza msimamo na kutenganisha masuala ya kijamii na masuala ya kisiasa na kiusalama, kama vile kuziunganisha tena familia.  

Ban amesema utata kati ya mataifa hayo mawili ya Korea umekuwa ukiongezeka, huku uhusiano wao ukisalia kuwa mbaya kwa muda mrefu sana. Amesema hatua hiyo basi ni ishara na mwelekeo mwema, na kuzihimiza pande hizo mbili kuendeleza kasi hiyo kwa kuendelea kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu, na kuchukua hatua za kujenga kuaminiana.

Ameelezea pia utashi wake mkubwa wa kuchangia kuendeleza amani, maendeleo na utulivu kwenye rasi ya Korea na pia kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.