Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aalika Iran na nchi nyingine 9 kushiriki kongamano kuhusu Syria

Ban aalika Iran na nchi nyingine 9 kushiriki kongamano kuhusu Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, ametangaza leo kuwa ametoa mwaliko kwa mataifa mengine kumi, ikiwemo Iran, kushiriki kongamano la kimataifa kuhusu Syria hapo kesho Januari 20, mjini Montreux, Uswisi. Nchi nyingine zilizoalikwa kushiriki ni Australia, Bahrain, Ubeljiji, Ugiriki, The Holy See, Luxembourg, Mexico, Uholanzi na Jamhuri ya Korea.

“Naamini kupanua uwepo wa jamii ya kimataifa siku hiyo itakuwa ishara muhimu ya mshikamano kabla ya kazi ngumu ambayo ujumbe wa serikali ya Syria na upinzani utaanza kufanya siku mbili baadaye mjini Geneva.  Kama nilivyosema mara kwa mara, naamini kuwa Iran inatakiwa kuwa sehemu ya suluhu kwa mzozo wa Syria.”

Bwana Ban amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa kongamano hilo ni fursa ilosubiriwa kwa muda mrefu ya kumaliza machafuko na kuanza kuikarabati tena Syria. Amekaribisha uamuzi wa kundi la muungano wa upinzani kushiriki katika kongamano hilo, akisema anatazamia kuona uakilishi jumuishi wa upinzani.

Ban amesema baada ya takriban miaka mitatu ya uharibifu na mauaji na miezi mingi ya majadiliano kuhusu kongamano hilo, ni wakati wa pande zinazozozana Syria na jamii ya kimataifa kuungana na kuunga mkono suluhu la kisiasa, kutokana na matokeo ya mkutano wa kwanza wa Geneva.

“Natoa wito kwa wote wanaokuja Montreux kutekeleza majukumu yao kwa nia nzuri. Acha niweke hili dhahiri. Montreux siyo mahali pa mazungumzo. Makundi ya Syria yenyewe yataanza harakati hizo mjini Geneva mnamo tarehe 24 Januari. Mjini Montreux, tunakusanyika kuonyesha mshikamano wetu na harakati hizi na watu wa Syria ambao wameteseka sana. Ningependa kuzihimiza pande husika za Syria zenyewe kutilia maanani lengo moja: kumaliza madhila ya watu wa Syria na kuanza kwa mpito wa kufikia Syria mpya.”