Ban aweka matumaini ya Syria huko Geneva, kambi ya Yarmouk yapaziwa sauti

17 Januari 2014

Wakati macho na masikio yataelekezwa huko Uswisi wiki ijayo kwenye mkutano wa pili wa kimataifa juu ya amani ya Syria, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema tukio hilo ni fursa pekee ya kuleta amani nchini humo.

Amekaririwa akisema ni matumaini yake pia suala la mamlaka za mpito litatekelezwa kwa mujibu wa makubaliano ya Geneva ya mwezi Juni mwaka 2012. Wakati huo huo mashirika ya kimataifa ya usaidizi ikiwemo UNRWA yametaka washiriki wa mkutano huo kuondoa vikwazo kwenye kambi ya wakimbizi ya Yarmouk nchini Syria ili vifaa vya usaidizi viweze kufikia walengwa.

Wito huo umekuja wakati huu ambapo wakimbizi Elfu 18 kwenye kambi hiyo wamenasa katikati ya mapigano bila huduma za msingi. Kinachohojiwa ni hadi lini wanawake na watoto kwenye kambi hiyo wataendelea kuteseka wakati wa uzazi bila huduma za tiba.