Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali nchini Mali

Baraza la Usalama lajadili hali nchini Mali

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili hali nchini Mali, ambapo pia limesikiliza ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu hali nchini humo. Joshua Mmali na taarifa kamili

(TAARIFA YA JOSHUA)

Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kwenye Baraza la Usalama, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Mali na Mkuu wa ujumbe wa kuweka utulivu nchini humo, MINUSMA, Albert Koenders, amesema masuala ya kipaumbele katika kurejesha utulivu na usalama nchini Mali yalishatambuliwa, na kile kinachohitajika sasa ni uungwaji mkono kikamilifu wa jamii ya kimataifa.

Bwana Koenders amesema ili kupiga hatua katika masuala hayo, ambayo ni maridhiano ya kitaifa, kuwawajibisha wanaotenda uhalifu na ufisadi, pamoja na kuimarisha taasisi za kitaifa na uongozi, Mali itahitaji kuchukua fursa iliyopo ya kipekee, na kuungwa mkono na jamii ya kimataifa katika miezi michache ijayo, ili kukabiliana na vianzo kanganishi vya mizozo nchini humo.

Changamoto za kiusalama na matarajio ya raia wa Mali ni makubwa. Kwa hiyo ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kuendelea kuunga mkono, bila kuchelewa, juhudi za kuongeza kasi ya kutoa na kupeleka vikosi vya MINUSMA vilivyosalia kaskazini mwa nchi.

Bwana Konders amesema hatua zimepigwa katika masuala ya kibinadamu, kufuatia juhudi za serikali ya Mali, ambayo ameishukuru katika kuunga mkono operesheni za kibinadamu. Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto kubwa kwa mwaka 2014, kwani takriban watu nusu milioni bado hawajarejea makwao.