Nimejizatiti kuimarisha uwezo wa UNMISS katika kulinda raia Sudan Kusini: Ban

23 Disemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezungumza na waandishi wa habari mjini New York hii leo kuhusu mzozo wa kikabila unaoendelea nchini Sudan Kusini na kusema kuwa leo anaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa raia nchini humo wanalindwa. Ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kulishirikisha baraza la usalama.

(Sauti ya Ban)

“Karibu siku nzima ya leo nitatumia kuwasiliana na viongozi wa kikanda na wengine kuwasihi waongeze uwezo wa kijeshi kwa UNMISS pamoja na ushawishi wa kisiasa kumaliza mgogoro huo. Halikadhalika leo nitawasilisha barua kwa baraza la usalama yenye mapendekezo yangu kuhusu jinsi ya kuimarisha uwezo wa UNMISS kulinda raia kwa kupatiwa askari zaidi, polisi na vifaa vinginevyo. Tayari tunawasiliana na nchi nyingine kusaidia kukidhi mahitaji hayo. Pia tunaangalia vikosi vingine vya kulinda amani bila kuathiri uwezo wao wa kiutendaji kule wanakofanya operesheni zao.”

 

Bwana Ban akaweka bayana kuhusu suala la ulinzi wa raia na ukiukwaji wa haki za binadamu.

(Sauti ya Ban)

Hebu niweke bayana, dunia inatazama pande zote Sudan Kusini. Mashambulizi dhidi ya raia na walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliotumwa kuwalinda yanapaswa kusitishwa mara moja. Umoja wa Mataifa utachunguza ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu na uhalifu dhidi ya binadamu. Wahusika katika ngazi ya juu watawajibishwa hata kama watadai kuwa hawakufahamu vitendo hivyo vikifanyika. Nimezungumza mara kadhaa na Rais Salva Kiir na viongozi wa upinzani na kuwataka waende kwenye meza ya mazungumzo. Tofauti zozote zilizopo haziwezi kuhalalisha ghasia iliyokumba taifa hili changa.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter