Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

M23 tumeshawang’oa, sasa ni FDLR, asema Kobler kwa Baraza la Usalama

M23 tumeshawang’oa, sasa ni FDLR, asema Kobler kwa Baraza la Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa kuweka utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, Martin Kobler, ametangaza kuwa baada ya kuwang’oa waasi wa M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, sasa mapambano yanawageukia waasi wa FDLR.

Hayo yamesemwa na rais wa Baraza la Usalama mwezi huu, Balozi Gerard Araud wa Uafaransa katika mkutano na waandishi wa habari

(SAUTI YA ARAUD)

“Bwana Kobler ametangaza kuanzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya FDLR. Ameeleza pia kuwa operesheni hiyo haiwezi kuwa sawa na ile dhidi ya M23, kwani M23 walikuwa wanapigana vita vya kawaida, wakiwa na wanajeshi wenye silaha wanaoweza kutambuliwa kwa urahisi, lakini FDLR ni makundi madogo madogo yanayoishi katika vijiji vidogo na familia zao, ikimaanisha, miongoni mwa raia, kwa hiyo itakuwa operesheni ngumu sana. Hata hivyo, operesheni hiyo itaendelea bila kusita.”

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya Balozi Araud, Bwana Kobler amesema hali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imebadilika baada ya kuhitimisha makabiliano na waasi wa M23. Ameongeza kuwa, ingawa bado baadhi ya raia wanasita kuamini kuwa utulivu umerejea, maeneo mengi yamekombolewa, na hali ya utulivu inayorejeshwa sasa haiwezi tena kusambaratika kwa urahisi.

Hata hivyo, ameongeza kuwa ili kudumisha utulivu huo, ufanisi wa kijeshi pekee hautoshi

“Inahitaji hususan hatua mathubuti za raia, Raia washikamane, wadai na kupata huduma za afya, elimu, kuwa na amani na usalama, udhibiti wa madini, ambayo ni sehemu ya vyanzo vya migogoro, ili kukabiliana na matatizo yote. Bila hayo, ufanisi wa kijeshi utafeli na tutarejea tulikotoka. Ufanisi wa kijeshi ni muhimu, lakini juhudi za kiraia za kurejesha mamlaka za kitaifa, kuwa na demokrasia na uchaguzi, hayo yote ni muhimu.”

Kufuatia hotuba za Bi Mary Robinson, Bwana Herve Ladsous na Bwana Martin Kobler kwa Baraza hilo, Balozi Gerard Araud ameelezea leo kuwa siku ya furaha kuu kwa Baraza hilo

(SAUTI YA ARAUD

Hotuba ambazo zimetolewa kwa Baraza la Usalama na Bi Robinson, Bwana Kobler na Bwana Ladsous, zimepewa tuzo ya kuwa hotuba zenye matumaini zaidi za mwaka 2013, baada ya ufanisi dhidi ya M23, kuna msukumo mpya. Wakati huo huo, hakuna anayedanganyika, kwani alivyosema Bwana Kobler, ni ufanisi hafifu."