Israel kusafirisha vifaa vya ujenzi wa miradi ya UM Gaza:Serry

9 Disemba 2013

Mratibu maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu Mashariki ya Kati Robert Serry amethibitisha kwamba serikali ya Israel imeamua kuanza kusafirisha vifaa vya ujenzi kwa ajili ya miradi ya Umoja wa Mataifa Gaza.

Umoja wa Mataifa unaendesha ujenzi wa miradi muhimu yenye thamani ya dola milioni 500 Gaza ikiwemo shule,makazi, maji na usafi. Bwana Serry amesema Umoja wa mataifa utaendelea kulinda hadhi yake katika kazi hizo bila kuingiliwa na kwa uwazi kwa mujibu wa taratibu zilizoafikiwa.

Hata hivyo amesema hali Ukanda wa Gaza bado ni ya kutia hofu na Umoja wa Mataifa unajihusisha na pande husika kujaribu kushughulikia masuala muhimu na ya haraka kama umeme, maji, na ujenzi wa sekta binafsi.

Ameongeza kuwa Umoja wa mataifa unatumai kwamba suluhu itapatikana haraka ya matatizo haya hususan la umeme na kutoa wito wa msaada wa jumuiya ya kimataifa katika suala hili kwani amesema wakati ni sasa.