Baraza la usalama lamulika LRA

25 Novemba 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja limelaani vikali vitendo vya mashambulizi na uhalifu wa kivita vinavyotekelezwa na waasi wa Lord’s Resistance Army, LRA, pamoja na kupitisha azimio la kuongeza muda wa kuhudumu kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kuweka utulivu Abyei. Joshua Mmali na taarifa kamili.

(Taarifa ya Joshua)

Katika taarifa ya rais wa Baraza la Usalama, wanachama wa Baraza la Usalama wamelaani uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaotekelezwa na waasi wa LRA, pamoja na ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo la Afrika ya Kati.

Baraza hilo pia limelaani vitendo vya LRA kuwateka na kuwatumia watoto katika vita, mauaji, ubakaji, utumwa wa kingono na vitendo vingine vya ukatili wa kingono, na kuwataka waasi hao kuwaachilia huru mara moja watu walotekwa nyara na kujisalimisha.  Balozi Liu Jieyi wa Uchina ni rais wa Baraza hilo mwezi huu wa Novemba:

“Nawashukuru wanachama wa Baraza hili kwa mchango wao wa kuthaminiwa kwa taarifa hii. Kulingana na maafikiano yalofikiwa na wanachama wa Baraza hili, naamini kuwa wanachama wa Baraza hili wanaikubali taarifa hii. Imeamuliwa hivyo!”

Baraza la Usalama pia limekaribisha hatua zilizopigwa hivi karibuni katika kukomesha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaotekelezwa na LRA katika Afrika ya Kati, na kusisitiza azma yake ya kuendeleza kasi ya kuhakikisha tishio la LRA kwa usalama linaondolewa daima.

Wakati huo huo, Baraza la Usalama pia limepitisha azimio la kuongeza muda wa vikosi vya kuweka utulivu katika jimbo la Abyei, linalozozaniwa kati ya Sudan na Sudan ya Kusini kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi. Wakiongea baada ya azimio hilo, wawakilishi wa kudumu wa Sudan na Sudan Kusini wamelishukuru Baraza hilo, na Ethiopia kwa kuchangia vikosi hivyo vya amani