Jamhuri ya Korea yaupiga jeki mfuko wa Global Fund

21 Novemba 2013

Mfuko wa Kimataifa kwa ajili ya kupanbana na Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria, umekaribisha tangazo la Jamhuri ya Korea kuwa itaongeza maradufu mchango wake kwa mfuko huo wa Global Fund kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa kutumia fedha zitakazotokana na ada inazotoza wanunuzi wa tikiti za safari za ndege.

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Korea imesema kuwa itachangia dola milioni 6 kwa mfuko wa Global Fund kati ya mwaka 2014 na 2016.

Dola milioni 10 zaidi zitokanazo na ada wanayolipa wasafiri wote wanaoondoka Korea kwenye safari za kimataifa, zitatolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea kwa Global Fund katika mafungu matano tofauti ya dola milioni mbili kila mwaka, kuanzia mwaka huu wa 2013 hadi 2017.

Akikaribisha tangazo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Global Fund, Mark Dybul amesema kuwa Jamhuri ya Korea imetoa mfano wa kuigwa katika kutumia mbinu bunifu kukabiliana na magonjwa hayo matatu. Amesema, kwa kuongeza mchango wake maradufu, Korea inatoa uongozi kwa mataifa mengine yaloendelea ya G20 kufuata nyayo zake.