Baraza la Usalama laongeza muda wa AMISOM nchini Somalia

12 Novemba 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na vikao vya wazi na faragha vikimulika hali ilivyo nchini Somalia wakati huu ambapo serikali inajitahidi kuimarisha usalama ili shughuli za maendeleo ziweze kufanyika. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Novemba Balozi Liu Ji Ye kutoka China akiashiria kuanza kwa kikao kuhusu Somalia na hapa ajenda hapa ikiwa hatma ya uwepo wa vikosi vya Muungano wa Afrika nchini humo AMISOM, vikosi ambavyo awali muda wake ulikuwa umalizike Februari 2014 lakini sasa, wajumbe wamepitisha azimio na kuongeza miezi Minane zaidi hadi Oktoba 2014. 

Halikadhalika wajumbe wametaka idadi ya askari wa AMISOM iongezwe kutoka zaidi ya Elfu 17 sasa hadi 22,126 kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  Wametambua kuwa mazingira bado si sahihi kupeleka walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa huku wakiazimia kuongeza usaidizi wa vifaa kwa AMISOM.

Mwakilishi wa kudumu wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Dk. Elmi Ahmed Duale akapata fursa ambapo alishukuru Baraza la Usalama kwa kuwa bega kwa bega na Somalia na kuimarisha AMISOM lakini akatanabaisha suala la uwezeshaji jeshi la Somalia…

(Sauti ya  Balozi Duale)

 Tunataraji kwamba jeshi la Somalia linalopigana  bega kwa bega na AMISOM dhidi ya masalia ya ngome za Al Shabaab nao pia watapata msaada stahili, endelevu na kwa wakati muafaka kupitia mifuko ya Umoja wa Mataifa.”