Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aendelewa kutiwa hofu na athari za kimbunga nchini Ufilipino:

Ban aendelewa kutiwa hofu na athari za kimbunga nchini Ufilipino:

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amesema anaendelea kutiwa hofu na athari za kimbunga Haiyan ambacho ni moja ya vimbunga vikubwa kuwahi kutokea. Kimbunga hicho kimeathiri takriban watu milioni 9.5 nchini Ufilipino , huku kikisababisha uharibifu mkubwa , kutawanya watu na ukatili maisha ya watu wengi wakati idadi ya waliokufa ikitarajiwa kuongezeka. Hivi sasa misaada imeanza kuwasili katika maeneo ya vijijini.

Ban amezungumza na balozi wa Ufilipino kwenye Umoja wa mataifa Libran N. Cabactulan, kumwambia Umoja wa Mataifa uko tayari kuwasaidia watu wa Ufilipino na serikali ya nchi hiyo katika kipindi hiki kigumu cha kukabiliana na athari za kimbunga. Katibu Mkuu amesema mashirika ya Umoja wa mataifa na washirika wake wanaendelea kutoa misaada ya dharura ili kuzisaidia familia ambazo zinahitaji msaada huo.

Hata hivyo amesema bado kuna sehemu ambazo ni vigumu kuzifikia kwani barabara zimeharibiwa vibaya , viwanja vya ndege na madaraja yamesambaratishwa au kushindwa kupitika kwa ajili ya vifusi. Mashirika yameanza kupeleka kwa helkopta na ndege chakula, madawa, vifaa vya malazi na vitu vingine vya kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na kupeleka timu ya wataalamu kutoa misaada muhimu ya kiufundi.

Ban amewashukuru nchi wanachama kwa kujitoa kwao ikiwa ni pamoja na msaada wa fedha , timu za misaada na msaada wa kijeshi. Ameitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea kuonyesha mshikamano kwa watu wa Ufilipino.