Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanamuziki wa Uchina, Lang Lang atangazwa kuwa Balozi Mwema wa Amani

Mwanamuziki wa Uchina, Lang Lang atangazwa kuwa Balozi Mwema wa Amani

Umoja wa Mataifa una balozi mpya wa amani. Jina lake, ni Lang Lang, mcheza kinanda maarufu kutoka Uchina.

 [Muziki]

Na huo, ni mdundo uitwao Chopin Waltz, uloendana na hafla ya kumsimika balozi mwema wa amani. Aliyemtangaza, ni Katibu Mkuu, Ban Ki-moon

 “Kwa furaha na fahari, namtangaza Lang Lang kama balozi mwema wa amani wa Umoja wa Mataifa. Lang Lang, hongera na nakutakia kazi njema kwa ajili ya amani ya dunia!”

Katika ujumbe wake, Bwana Ban alisema muziki una uwezo mkubwa wa kufungua mioyo na fikra za watu

“Kupitia utani wake, na kipaji chake kikubwa, Lang Lang anawaunganisha watu, siyo tu kupitia kwa muziki wake, bali pia katika shauku yake ya kujenga ulimwengu bora zaidi kupitia katika elimu. Najua ujumbe wa Lang Lang utasambaa kutoka kumbi za burudani hadi kwenye kumbi za shule.”

Akiiipokea beji ya ubalozi wema, Lang Lang alielezea furaha yake

“Ni kwa unyenyekevu mkubwa leo napokea beji hii ya kipekee. Naahidi kufanya kila niwezalo, nikisafiri kote duniani kuongeza ufahamu kuhusu mkakati wako wa kimataifa wa Elimu Kwanza. Watoto na muziki ndio hunipa shauku. Natumai nitawachagiza watoto kuwa na ndoto.”

Lang Lang, anajiunga kwenye orodha ya mabalozi kumi na mmoja wema wa amani, wakiwemo mwanamuziki mashuhuri Stevie Wonder na mwigizaji filamu George Clooney.

 [Muziki]