Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

NEPAD ndio muarobaini wa maendeleo barani Afrika: Baraza Kuu

NEPAD ndio muarobaini wa maendeleo barani Afrika: Baraza Kuu

Wiki ya Afrika katika Umoja wa Mataifa imefikia kilele Ijumaa kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujadili mpango mpya wa ushirikiano wa maendeleo barani humo, NEPAD wakimulika zaidi mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake na jinsi ya kuimarisha ushirikiano huo. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Mjadala wa wazi kuhusu NEPAD na harakati za kuchagiza usaidizi ili iweze kufanikiwa ulianza kwa hotuba ya Rais wa baraza hilo Balozi John Ashe iliyosomwa na mwakilishi wa kudumu wa Timor letse Sofia Borges ambayo ilitambua vile ambavyo mafanikio ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika baadhi ya nchi za Afrika yalivyochochewa na NEPAD.

Hata hivyo amesema bado kuna changamoto lakini NEPAD ndio suluhu iwapo itaungwa mkono kitaifa na kimataifa. Amekariri ripoti ya Katibu Mkuu inayosema kuwa baadhi ya nchi za Afrika ziko mashakani kufikia malengo ya milenia hivyo akasema..

(Sauti ya balozi Borges)

“Kwa muda uliobakia kabla ya ukomo mwaka 2015, tunapaswa kuongeza kasi na kushawishi utashi wa kisiasa. Na tunavyoandaa ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, baraza kuu litahitaji kuweka mkazo kuona vipi ajenda hiyo inahusiana na Afrika. Vipaumbele vya maendeleo vya Afrika kama vilivyoainishwa kwenye NEPAD vijumuishwe vyema kwenye ajenda hiyo mpya.”