Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yajikita kurejesha vitambulisho kwa wakimbizi wa Syria

UNHCR yajikita kurejesha vitambulisho kwa wakimbizi wa Syria

Nchini Jordan, wafanyakazi wapatao 50 wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR wanafanya kazi kutwa kucha ili kukamilisha kazi ya kurejesha vitambulisho kwa wakimbizi wa Syria ambao walivisalimisha wakati kabla ya kuingia kambi ya Za’atari nchini Jordan. Kazi hiyo inayofanyika kituo cha Raba'a al-Sarhan kilicho mpakani mwa nchi mbili hizo, inafuatia makubaliano ya mwezi Julai mwaka huu kati ya serikali yaJordanna UNHCR ya kutaka vitambulisho hivyo virejeshwe kwa wahusika kwa kuwa wanavitaka kwa sababu moja hadi nyingine. Hata hivyo kazi hiyo imekuwa ngumu kutokana na mlundikano wa nyaraka hizo baada ya wakimbizi wengi kukimbia machafuko nchiniSyriana kusababisha mfumo wa kupokea nyaraka na kuhifadhi kuzidiwa uwezo. Mkuu wa operesheni za UNHCR nchini Jordan Andrew Harper amesema pamoja na kwamba kazi hiyo ni ngumu, wanapata faraja na furaha kubwa pindi wanapoweza kuwarejeshea wakimbizi hao nyaraka zao na furaha hujidhihirisha usoni. UNHCR inasema wigo wa urejeshaji utahusisha pia wakimbizi walio kambini na pia ina mpango wa kuanzisha kazi ya kusajili upya wakimbizi ili kupata idadi kamili na hivyo kurahisisha kazi ya utoaji misaada na huduma kwa wakimbizi hao.