Kazi ya udhibiti wa silaha za kemikali Syria yaanza rasmi

2 Oktoba 2013

Huko Damascus hii leo, jopo linaloendesha operesheni ya kuhakikisha Syria inaondokana na mpango wake wa silaha za kemikali ifikapo katikati mwa mwaka ujao, limekalisha siku ya kwanza ya kazi hiyo. Katika siku hiyo ya kwanza, jopo hilo linalojumuisha wataalamu kutoka shirika la kudhibiti silaha za kemikali, OPCW na Umoja wa Mataifa limeshirikiana na mamlaka za Syria kutambua maeneo husika yenye silaha hizo ambako jopo hilo litafanya kazi na pia mambo ya kufanya kukabiliana na athari za kiafya na kimazingira ambazo watakabiliana nazo.

Mipango pia inaendelea ili kutekeleza jukumu la haraka zaidi la kuharibu mitambo ya utengenezaji wa silaha hizo huku majadiliano yakiendelea kuhusu ukubwa wa silaha zilizohifadhiwa. Katika majadiliano hayo pande hizo zimesisitiza juu ya umuhimu wa Syria kuzingatia ukomo wa kuthibitisha na kuharibu silaha ilizo nazo. Hata hivyo ilielezwa bayana kuwa jopo hilo litatoa usaidizi ili Syria iweze kuhakikisha inatekeleza kabla ukomo haujafikia.