Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumza na Mwakilishi wa EU kuhusu hali Misri

Ban azungumza na Mwakilishi wa EU kuhusu hali Misri

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Mwakilishi Mkuu wa masuala ya nchi za nje wa Jumuiya ya Ulaya, EU, Catherine Ashton, kufuatia ziara yake nchini Misri.

Bwana Ban ameelezea wasiwasi wake kuhusu mkondo ambao kipindi cha mpito nchini Misri kimefuata, na hasa kuhusu kutiwa kwa watu rumande nchini humo, akiwemo rais wa aliyepinduliwa, Mohammed Morsy. Katubu Mkuu amesema ni vyema kwamba mwakilishi huyo mkuu wa EU alikuwa amemwona Bwana Morsy, na kurejelea wito wake wa kuachiliwa kwa Bwana Morsy na maafisa wa chama cha Muslim Brotherhood.

Katika mazungumzo hayo ya simu, wamesisitiza umuhimu wa kuwa na harakati jumuishi za kisiasa, ambazo zitawakilisha maoni na matakwa ya kila pembe ya uwanja wa kisiasa nchini Misri. Mbali na Misri, wamejadili pia harakati za amani ya Mashariki ya Kati, ambapo Katibu Mkuu ameelezea matumaini yake kuwa juhudi za sasa za kuwaleta Waisraeli na Wapalestina kwenye meza ya mazungumzo zitafanikiwa, na kuahidi msaada wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine.