Serikali ya Syria imeruhusu waangalizi wetu kuendesha mambo kwa uhuru-Ban

15 Agosti 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa serikali ya Syria hatimaye imekubali rasimi kutoa ushirikiano kuwezesha timu ya waangalizi kuendesha majukumu yake katika mazingira safi, salama na katika hali ya ufanisi.

Amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulioko nchini humo sasa unaweza kuondoka katika muda wowote muafaka. George Njogopa na maelezo zaidi.

(Taarifa ya George)

Katika taarifa yake, Ban amesema kuwa, amekubaliana na serikali ya Syria kuwa timu hiyo ya wajumbe itaendelea kusalia nchini humo kwa kipindi cha siku 14 ili kuendelea na majukumu yake ikiwemo yale yanayohusu kutembelea maeneo mbalimbali.

Amesema kuwa, ametiwa moyo na hatua hiyo hivyo anapenda kutuma shukrani zake za dhati wa serikali ya Syria. Kwa upande mwingine Ban ameihakikishia Damascus kuwa ujumbe huo utafanya kazi zake kwa welidi na bila kuegemea upande wowote .

Ujumbe wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa umeelekea nchini humo kwa ajili ya kuendesha uchunguzi kuhusu uwezekano wa kuwepo matumizi ya kemikali za sumu wakati wa mapigano baina ya vikosi vya serikali na vikosi vya wanamgambo ambao wanaupinga utawala wa Assad.

Ban ameongeza kusema kuwa amevutiwa na namna Jumuiya ya Kimataifa ilivyounga mkono suala la kutumwa kwa wajumbe hao akisema kuwa hatua hiyo inaonyesha kuwa matumizi ya silaha za kemikali kwa njia yoyote ni uhalifu wa kipindukia.