Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pakistan na Afghanistan zaathirika na mvua nzito na mafuriko: OCHA

Pakistan na Afghanistan zaathirika na mvua nzito na mafuriko: OCHA

Mvua nzito nchini Pakistan zimesababisha vifo vya watu wapatao 58 na na majeruhi kwa watu 30, kwa mujibu wa mamlaka ya udhibiti wa majanga nchini humo. Wakati huo huo, vijiji 13 vimeathiriwa na mafuriko nchini Afghanistan. George Njogopa na taarifa kamili:

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Mvua hiyo pia imeleta uharibifu mkubwa katika maeneo mengine ikiwemo kusababisha mamia ya watu kukosa makazi baada ya nyumba zao kuharibiwa.Mashamba pamoja na miundo mbinu ni baadhi ya maeneo mengine ambayo pia yamevurugwa na mvua hiyo.

Ripoti zinasema kuwa, mvua inazidi kuendelea na taarifa za watabiri wa hali ya hewa zinaonyesha kwamba kiwango cha mvua hiyo kinatazamiwa kuongezeka katika kipindi cha mwezi huu wa Ogosti. Serikali ya Pakistan tayari imeanzisha jitihada za uokozi kwenye maeneo yaliyoathiriwa  lakini hata hivyo haijaonyesha dalili ya kuomba msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Mashirika ya kimataifa ya utoaji msaada wa usamaria mwema ikiwemo lile la OCHA yamesema kuwa yanaendelea kufuatilia kwa karibu hali ilivyo nchini humo, na pindi itapoona kuna ulazima wa kutoa msaada itafanya hivyo mara moja.  UM watilia shaka ustawi wa watoto walioko kwenye makambi nchini Syria. Umoja huo umesema kuwa makambi mengi yanayohifadhi watoto nchini Syria yanatia shaka kwani mengi yao hayana ulinzi huku wengine wakilazimika kujiingiza kwenye kazi ili kuzisaidia familia zao.

Kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, baadhi ya watoto wa kike wanaolewa wakiwa katika umri mdogo na wengine wanachukuliwa na kuingizwa kwenye makambi ya kijeshi na kugezwa wapiganaji. Mashirika hayo lile la kuhudumia watoto UNICEF na lile linalohusika na wakimbizi UNHCR yameanzisha juhudi za kutambua matatizo hayo ili hatimaye kuyatafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake UNHCR imesema kuwa inafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha kwamba wanawake wajawazito wanafikiwa na huduma bora za kiafya wakati wa kujifungua.