Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wakimbizi Elfu 10 wa Ivory coast waondoshwa Liberia

Zaidi ya wakimbizi Elfu 10 wa Ivory coast waondoshwa Liberia

Shirika la kuhudumia wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, UNHCR linasema kuwa zaidi ya raia Elfu Kumi wa Ivory Coast waliokimbilia Liberia miaka miwili iliyopita kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi wamerejea nyumbani mwaka huu. Assumpta Massoi na taarifa kamili.(TAARIFA ASSUMPTA)

Wakimbizi hao wengi wao walikuwa wakiishi kwenye kambi na kaya za wenyeji huko Grand Gedeh, Nimba, Maryland na Mto Gee nchini Liberia wanarejea makwao kufuatia uratibu unaofanywa na UNHCR na tume ya kurejesha wakimbizi ya Liberia.

Afisa wa UNHCR Andrew Mbogori amesema mwaka jana waliwezesha wakimbizi zaidi ya 5,700 kurejea nyumbani na mwaka huu mpango ni kurejesha wakimbizi Elfu Kumi na sita, ambapo tayari Elfu Kumi kati yao wamerejea mwaka huu pekee.

Amesema mwaka jana zoezi hilo lilikwamishwa na ukosefu wa usalama mpakani lakini kwa sasa hali ya usalama imeimarika. Hata hivyo ametaja changamoto mpya kuwa ni miundombinu ya barabara kutokana na mvua lakini wanashirikiana na wadau kuimarisha barabara ili zoezi liendelee. Pindi baada ya kurejea nyumbani wakimbizi hao hupatiwa mikopo ya fedha na misaada ya vyakula na vifaa muhimu. Liberia inahifadhi zaidi ya wakimbizi Elfu 58 kutoka Ivory Coast.