Kulinda waandishi wa habari ni kulinda haki na demokrasia: Eliasson

17 Julai 2013

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Jan Eliasson, leo amesema hatua inayopaswa kuchukuliwa kila mwandishi wa habari anapouawa, ni kuhakikisha mauaji hayo yamechunguzwa na haki kutendeka. Akilihutubia Baraza la Usalama ambalo limekutana kujadili ulinzi wa raia na hususan waandishi wa habari, Bwana Eliasson amesema inashangaza na haikubaliki kuwa zaidi ya asilimia 90 ya mauaji ya waandishi wa habari hufanyika bila kuwajibisha wanayoyatekeleza kisheria."Tukumbuke kwamba kila wakati mwandishi wa habari anapouawa na watu wenye msimamo mkali, walanguzi wa madawa ya kulevya au hata vikosi vya serikali, sauti moja huondolewa kwa sauti zinazopaziwa waathiriwa wa mizozo, uhalifu na ukiukwaji wa hki za binadamu. Kila mwandishi wa habari anayeuawa au kunyamazishwa kwa kutishwa, humaanisha shahidi mmoja wa juhudi za kulinda haki na kuhakikisha heshima ya ubinadamu.”

Bwana Eliasson amesema wengi wa waandishi habari ambao huuawa huwa wanafuatilia habari za ufisadi na vitendo vingine vya uhalifu, na wengi wao huwa ni wenyeji wa nchi wanakofanyia kazi. Naibu Katibu Mkuu amesema ulinzi wa vyombo huru vya habari ni msingi wa haki ya kujieleza na demokrasia.

Mkutano huo wa Baraza la Usalama umehudhuriwa na waandishi wawili wa habari- wakiwemo Mustafa Haji Abdinur kutoka Somalia, na Ghaith Abdul-Ahad kutoka Iraq.