Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cameroon imeendeleza haki za binadamu lakini bado kuna upungufu: Pillay

Cameroon imeendeleza haki za binadamu lakini bado kuna upungufu: Pillay

Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema tathmini ya ukaguzi ulofaywa nchini Cameroon imeonyesha nchi hiyo kupiga hatua katika kuimarisha haki za binadamu. Hata hivyo, Bi Pillay ambaye amekamilisha ziara yake nchini humo amesema bado kuna hali zinazosikitisha, kama vile dhuluma dhidi ya wanawake, kuwatelekeza waandishi wa habari, kuhalifisha mapenzi ya jinsia moja na hatari dhidi ya jamii za kiasili, ambazo zinakabiliwa na matishio yatokanayo na shughuli za uchimbaji migodi na ukulima wa biashara.

Katika mkutano na waandishi wa habari mwishoni mwa ziara yake, Bi Pillay amesema haya ndiyo masuala aliyozungumzia katika mikutano yake na viongozi wa serikali, mashirika ya umma, na wawakilishi wa kidiplomasia.

Bi Pillay amesema hatua inayofuata kwa Cameroon, ni kuangazia utekelezaji wa mapendekezo ya mikataba ilowekwa katika ngazi mbalimbali, utaratibu maalumu na ukaguzi wa kila mara wa kimataifa, ili kuweka mfumo imara na jumuishi wa kulinda haki za binadamu kwa manufaa ya watu wote.