Twahitaji wachangiaji damu hiari: WHO

12 Juni 2013

Mahitaji ya damu yanaongezeka kila mwaka na mamilioni ya wanaohitaji huduma hiyo ili kuokoa maisha yao hawapati kwa wakati, na hiyo ni taarifa ya shirika la afya duniani, WHO katika kuelekea siku ya kimataifa ya uchangiaji damu kwa hiari tarehe 14 mwezi huu. WHO inasema mwaka 2011 walikusanya takribani michango hiari ya damu Milioni 83 duniani kote, ongezeko ambalo ni karibu Milioni Nane ikilinganishwa na mwaka 2004.  Kwa mantiki hiyo shirika hilo linatoa wito kwa mamlaka za afya duniani kuhamasisha watu kuchangia damu kwa hiari huku likisema kuwa damu inayotolewa kwa hiari ni salama zaidi na ina maambukizi machache ikilinganishwa na ile inayotoka kwa watu wanaotoa damu kwa malipo au ile inayotolewa na familia nyakati za dharura kwa ajili ya jamaa yao. Dkt. Neelam Dhingra, kutoka kitengo cha damu cha WHO anasema kuna takribani nchi 60 ambazo hukusanya asilimia 100 ya damuyaokutoka kwa wachangiaji damu kwa hiari na amesema ni vyema uchangiaji damu salama uwe sehemu ya sera ya taifa ya afya.

 (SAUTI YA Dkt,. Dhingra)

 

“Tukilinganisha takwimu za 2004 na 2011 kuna ongezeko la asilimia 35 la uchangiaji damu duniani kote lakini bado kuna uhaba mkubwa wa damu kwa mamilioni ya wagonjwa duniani kote hasa pale wanapokuwa wanaihitaji kwa dharura. Hivyo tunahitaji wachangiaji damu zaidi. WHO inasihi damu yote inayochangia ichunguzwe magonjwa ya ukimwi, homa ya ini, au Hepatits B, C na Kaswende. Nyongeza ya hiyo kuna magonjwa mengine ambayo WHO inapendekeza yachunguzwe kulingana na uwepo wake kwenye eneo husika kama vile Malaria, kansa ya damu na kirusi cha West Nile.”