Utapiamlo na utipatipwa miongoni mwa watoto ni tishio nchi zinazoendelea: WHO

6 Juni 2013

Shirika la afya duniani limetoa ripoti inayomulika vitisho viwili vya afya kwa watoto kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Afrika ikitaja kuwa ni utipwatipwa au uzito kupita kiasi na wakati huo huo ukosefu wa lishe bora. Taarifa ya Jason Nyakundi inafafanua zaidi.

 (TAARIFA YA JASON)

WHO inasema kuwa zaidi ya asilimia 75 ya watoto milioni 43 walio chini ya miaka mitano walio na uzito wa juu wanaishi kwenye nchi zinazoendelea hali ikizidi kuongezeka barani Afrika ambapo idadi hiyo imeongezeka maradufu kwa muda wa miaka ishirini iliyopita.

WHO inasema kuwa kuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha  kuwa watoto wasiopata lishe inayostahili  wakiwa wachanga  wanaweza kuwa na uzito wa juu wakikua na baadaye kuwa na magonjwa yasiyo na tiba.

Dr Francesco Branca kutoka idara ya lishe ya shirika la WHO anasema kuwa kuboreshwa kwa lishe kwa akina mama wajawazito na kuwashauri akina mama kunyonyesha watoto kunaweza kuzuia utapiamlo na uzito wa juu wa mwili.

 (SAUTI YA BRANCA)

“Kwa hali hizi zote tunajua kile kinachoweza kufanywa, ni jambo la kuwafikia walio na mahitaji. Tunahitaji kuchukua hatua zilizo nafuu na rahisi kuboresha lishe tangu utotoni. Mtoto akizaliwa ni lazima ihakikishwe kuwa lishe bora ipo. Kwa hivyo ni kunyonyesha kunastahli kufanywa tangu mwanzo na kuendelea kwa muda wa miezi sita ya kwanza na kuendelea hadi kwa kipindi cha miaka miwili. Wakati mtoto ashamaliza miezi sita ya kwanza hatua muhimu ni kuhakikisha kuwa kuna lishe iliyo bora na ya kila wakati  kupitia kwa chakula cha familia au kupitia kwa chakula kingine cha kutengezewa viwandani.”