Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laijadili Somalia

Baraza la Usalama laijadili Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo limejadili hali ya Somalia ambapo limejulishwa ya kwamba miezi minane baada ya kuundwa kwa serikali, mwelekeo ni mzuri licha ya kwamba serikali inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuunda taasisi thabiti za usalama, haki na kuweka fursa za kiuchumi kwa raia wake. Joshua Mmali na ripoti zaidi.

(TAARIFA YA JOSHUA)

Akiongea katika mkutano huo wa Baraza la Usalama, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson amesema Somalia bado inakabiliana na changamoto nyingi, lakini ni lazima kukumbuka ilokotoka nchi hiyo.

Bwana Eliasson amesifu mchango wa vikosi vya AMISOM na vile vya taifa hilo, pamoja na jamii ya kimataifa katika kuifikisha Somalia ilipo sasa, na kusema ufanisi huo unapaswa kutunzwa. Amesema wiki hii, hatua hata kubwa zaidi imepigwa kwa kuanzishwa ofisi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuisaidia Somalia, UNSOM

“UNSOM itasaidia katika mashauriano ya kisiasa, kujenga amani na kulinda haki za binadamu. Hata hivyo, ili kukabiliana na changamoto za kujenga amani kikamilifu kutategemea zaidi juhudi za serikali ya Somalia. Changamoto muhimu zaidi ni kuweka mfumo wa serikali unaotimiza majukumu yake. Nyingine ni uhusiano wa ushirikiano kati ya Somalia na jirani zake.”

Bwana Eliasson ameisifu serikali mpya ya Somalia kwa juhudi zake katika kuweka mipango ya maendeleo kisiasa, kujenga amani, na kuendeleza mazungumzo na taasisi za mikoa.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Somalia, Bi Fowsia Haji Yusuf Adan.

)