Nchi 36 za Afrika za laani matumizi ya mabomu mtawanyiko:

28 Mei 2013

Nchi 36 za Afrika zinazokutana nchini Togo zimelaani kuendelea na matumizi ya mabomu mtawanyiko duniani na kuyataka mataifa yote ya Afrika kutia saini mkataba wa kimtaifa unopinga mabomu hayo.

Katika taarifa yao iliyotolewa kwenye semina iliyoandaliwa mjini Lome kwa msaada wa shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP na serikali ya Norway wanasema mataifa ya Afrika yanahofia matumizi ya karibuni na yanayoendelea ya mabomu mtawanyiko duniani na athari zake. Wanasema matumizi ya mabomu hayo yamesababisha athari kubwa hususani kwa wanawake na watoto.

Taarifa hiyo imetoa wito wa kuacha mara moja matumizi ya mabomnu hayo na kuzitaka nchi za Afrika ambazo bado hazijasitisha kufanya hivyo na kuridhia mara moja mkataba wa kupinga matumizi ya mabomu mtawanyiko, mkataba ambao hadi sasa umesainiwa na mataifa 112.

Mkataba huo unapiga marufuku matumizi, uzalishaji, kuweka akiba, usafirishaji na utoaji msaada wa mabomu hayo. Nchi 12 za Afrika bado hazijaridhia mkataba huo. Mabomu hayo yanatumika katika nchi 24 na tawala tatu katika miaka ya karibuni.