Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA yalaani kutawanywa kwa wakimbizi wa Kipalestina Syria

UNRWA yalaani kutawanywa kwa wakimbizi wa Kipalestina Syria

Wakimbizi wa Kipalestina walioko nchini Syria wanauawa, kujeruhiwa na kutawanywa kwa kiasi kikubwa kuliko wakati mwingine wowote wakati vita vikiendelea kuwaathiri wakimbizi katika makambi yote nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA takribani wakimbizi wa Kipalestina 235,000 wametawanywa na machafuko ndani ya Syria. UNRWA inasema taarifa za Jummane zimezidi kutia hofu baada ya kuthibitishwa kwamba wakimbizi wengine 6000 wa Kipalestina wametawanywa katika kambi Ein El Tal iliyopo kilometa 12 kutoka mjini Aleppo Kaskazini mwa Syria.

Kufuatia miezi ya machafuko shirika hilo linasema mapambano baina ya waasi na majeshi ya serikali yameshuhudia katika kambi za wakimbizi huku magruneti na risasi zikiharibu makazi ya wakimbizi, kusababisha vifo na majeruhi ikijumuisha pia wakimbizi wa Kipalestina.

Wakati likiendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Kipalestina Syria UNRWA imelaani vikali mashambulizi ya makundi yenye silaha dhidi ya maeneo ya raia na kushindwa kwa pande zote kulinda maisha ya raia wa Syria na wakimbizi wa Kipalestina na hivyo kukiuka sheria za kimataifa za kulinda maisha ya watu na haki zao.