Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika lazima iboreshe bidhaa za viwandani ili kukuza uchumi na kumaliza umasikini

Afrika lazima iboreshe bidhaa za viwandani ili kukuza uchumi na kumaliza umasikini

Ripoti kuhusu hali ya uchumi barani Afrika inasema nchi za bara hilo zina fursa ya kuboresha na kubadili uchumi wake kwa kupitia bidhaa za viwandani kutokana na rasilimali nyingi zilizopo barani humo.Ripoti inasema Afrika itaweza kukabiliana na bei kubwa ya bidhaa kwa sasa na kubadili mfumo wa uzalishaji kimataifa, kama inavyofafanua zaidi ripoti hii ya Joshua Mmali.

(RIPOTI YA JOSHUA MMALI)

Sera kama hiyo ni muhimu, ikiwa bara la Afrika litataka kuwa thabiti kiuchumi na kuweza kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana, umaskini na pengo la usawa wa kijinsia, imesema ripoti hiyo kuhusu uchumi wa bara Afrika mwaka huu, ambayo imeandaliwa na Tume ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika na Tume na Muungano wa Afrika.

Mbali na kuongeza nafasi za ajira, vipato, na faida zitokanazo na kuongeza bei za bidhaa, ripoti inasema iwapo nchi za Afrika  zitaongeza thamani ya bidhaa kupitia viwandani, zitapata pia nafasi ya kupanua uwezo wao kiteknolojia, ujuzi wa kitaaluma na kuimarisha mifumoyaoya viwanda.

Licha ya kuwa na asilimia 12 ya utajiri wa mafuta kote duniani, asilimia arobaini ya dhahabu na utajiri wa madini mengine, pamoja na asilimia 60 ya ardhi yenye rutuba inayoweza kulimwa na rasilmali kubwa ya miti ya mbao, uwezo wa kuongeza thamani kwa bidhaa hizo bado ni haba, na hivyo, faida zitokanazo na mauzo ya bidhaa hizo ni duni mno.

Kwa mfano, asilimia 90 ya faida itokanayo na kahawa inayopandwa barani Afrika, inakwenda kwa nchi, Ulaya, Amerika Kaskazini na Asia.