Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wawili wa zamani wa Bosnia Herzegovina wafungwa miaka 22 jela

Viongozi wawili wa zamani wa Bosnia Herzegovina wafungwa miaka 22 jela

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu uliofanyika kwenye iliyokuwa Yugoslavia, ICTY huko The Hague, imewahukumu kifungo cha miaka 22 jela maafisa wa zamani wa ngazi ya juu wa Bosnia, Mićo Stanišić na Stojan Župljanin.

Wawili hao wamepatikana na hatia ya kutenda makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu kati ya mwezi Aprili na Disemba mwaka 1992 huko Bosnia-Herzegovina.

Ilithibitishwa kuwa Stanišić, akiwa Waziri wa mambo ya ndani ya Jamhuri ya Srpska alitenda uhalifu dhidi walitenda uhalifu dhidi ya binadamu katika manispaa 20 ilhali Župljanin, akiwa mkuu wa huduma za ulinzi huko Banja Luka alifanya uhalifu huo katika manispaa Nane.

Vitendo hivyo ni pamoja na mauaji, mateso kwa binadamu na kuwaweka watu katika mazingira yasiyo ya kibinadamu.

Mahakama hiyo ya ICTY tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993, imeshawafungulia mashtaka watu 161 ambapo kati yao watu 136 kesi zao zimehitimishwa.