MONUSCO yakaribisha kujisalimisha kwa Bosco Ntaganda

19 Machi 2013

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, umekaribisha kujisalimisha kwa Bosco Ntaganda, na uamuzi wa serikali ya Marekani kumsafirisha hadi The Hague, ambako anatakiwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ambao anadaiwa kuutenda katika eneo la Ituri kati ya 2001 na 2003.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Roger Meece, amesema kujisalimisha kwa Bosco Ntaganda na kuchukuliwa kwake kwa ICC kutasaidia kuendeleza harakati za amani katika DRC, na kutuma ujumbe mzito kwa wakiukaji wengine wa haki za binadamu kuwa hawapo juu ya sheria.

Bosco Ntaganda anakabiliwa na mashtaka ya makosa saba tofauti ya uhalifu wa kivita, na matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu. Pia, anadaiwa kuwatumia watoto katika vita vya silaha, vitendo vya mauaji, ubakaji na utumwa wa ngono. Kabla ya kujisalimisha, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa kundi la waasi la M23, mashariki mwa DRC.