Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Feltman asisitizia uchaguzi wa amani na uwazi nchini Kenya baada ya ziara yake Afrika

Feltman asisitizia uchaguzi wa amani na uwazi nchini Kenya baada ya ziara yake Afrika

Mkuu wa masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa, Jeffrey Feltman, leo ametoa wito kwa Kenya kufanya uchaguzi wa amani, uwazi na kwa njia ya kuaminika. Akikutana na waandishi habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Bwana Feltman amesema ziara yake nchini Kenya iliangazia uchaguzi huo wa tareje 4 Machi, na kurejelea ujumbe alioutoa kwa viongozi na raia wa Kenya.

Kuhusu Somalia, Bwana Feltman amesema taifa hilo la Pembe ya Afrika limepiga hatua kubwa kisiasa, lakini sasa kinachostahili kuzingatiwa ni kuteleleza katiba. Amesema Umoja wa Mataifa utabaki tayari kuisaidia Somalia kujenga tena mifumo ya uongozi wa kisheria, na kuzingatia masuala ya haki.

Amezungumza pia kuhusu ziara yake Burundi, akisema kuwa, ingawa nchi hiyo ilikuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe muongo mmoja uliopita, sasa inaendelea kuimarika, na hata kuchangia juhudi za amani kwingineko, kama vile nchini Somalia. Hata hivyo, amesadiki kuwa bado ina changamoto nyingi.

Kuhusu Mali, amesema kwamba Umoja wa Mataifa unaweka njia mpya na mifumo mipya ya kuchukua hatua zitakazofuata katika kukabiliana na suala la Mali. Baadhi ya mambo muhimu ni kuhakikisha kuwa hali ya usalama inaimarika, na kurekebisha hali ya kibinadamu.

Amesema, hata ikiwa njia ya kijeshi inachukuliwa kwa sasa, suluhu la kudumu kwa suala la Mali litakuwa la kisiasa, kwani mzozo huo umetokana na masuala muhimu ya kisiasa kama vile uchaguzi, ambayo ni lazima yazingatiwe ipasavyo.