UNICEF yataka watoto walindwe kwenye mgogoro unaoendelea Syria

29 Novemba 2012

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Anthony Lake amerejelea wito wake wa kutaka pande zote katika mgogoro nchini Syria kuhakikisha zinawalinda watoto nyakati zote.

Taarifa ya UNICEF imesema wito wa Bwana Lake unafuatia ripoti za wiki hii kutoka mashirika mbali mbali ikiwemo lile la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch ya kwamba watoto nchini Syria wanabakia vilema na hata kuuawa na mabomu ya rashasha yanayotumiwa kwenye mapigano hayo na wakati mwingine watoto kugeuzwa wapiganaji au walinzi.

Amesema vitendo hivyo vinasikitisha, ni vya aibu na haikubaliki kabisa kuona haki za watoto zinakiukwa kwa kiwango hicho.

Bwana Lake amesema iwapo hali hivyo itakavyoendelea, itazidi kuathri maisha ya sasa na ya baadaye ya watoto hao pamoja na Syria yenyewe.

Taarifa hiyo ya UNICEF imesema hivi sasa shirika hilo inashirikiana na Syria na nchi nyingine nne jirani kuwapatia maelfu ya watoto wa Syria pamoja na familia zao mahitaji muhimu.