OCHA yaongeza fedha kwa msaada huo Rakhine; WFP yaonyesha wasiwasi wa kuendeleza msaada mwaka ujao

27 Novemba 2012

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu OCHA kupitia mfuko wake wa utoaji misaada kwa dharura, CERF, imetoa nyongeza ya dola Milioni Tano nukta Tatu kwa ajili ya watu Elfu 36 waliopoteza makazi yao kutokana na ghasia za mwezi Oktoba kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar.

Fedha hizo zitasaidia jitihada za mashirika matano ya Umoja wa Mataifa na washirika wao kutoa huduma za afya, lishe, makazi, maji safi na salama, usafi na chakula kwa wakazi hao.

Hii ni awamu ya pili ya msaada wa OCHA kwa wakazi wa Rakhine kufuatia ghasia za kikabila za mwezi Juni na Oktoba mwaka huu.

Wakati huo huo, msemaji wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, Elizabeth Byrs amesema hadi sasa wameweza kupata fedha za kutosha kutoa msaada wa chakula huko Rakhine hadi mwisho wa mwaka huu, lakini akaonya kuwa wanaweza kusitisha msaada kwa kipindi cha mwaka mpya.

(SAUTI YA ELIZABETH BYRS)

WFP italazimika kuchukua fedha kutoka operesheni zake nyingine muhimu nchini Myanmar ili kuwezesha usambazaji wa dharura wa misaada huko Rakhine, iwapo hatutapata fedha nyingine haraka baada ya mwezi wa Disemba.”