Waasi wa kikundi cha M23 waingia mji wa Goma huko DRC: Msemaji UM

21 Novemba 2012

Waasi wa kikundi cha M23 wameripotiwa kuingia mji wa Goma, ulioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Eduardo Del Buey amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa hali katika mji wa Goma sasa ni mbaya na kwamba waasi hao wamekuwa wakisonga mbele licha ya wito wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja huo na hata Umoja wa Afrika wa mataifa mengine ya kuwataka waasi hao kuacha mapigano mara moja.

Bwana Del Buey amesema ripoti zinaonyesha kuwa waasi hao wameteka wanawake na watoto, wamepora na kuharibu mali na kuwatishia waandishi wa habari na watu wengine waliokuwa wanajaribu kukataa udhibiti kutoka kwa waasi hao.

Amesema kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kusimamia utulivu huko DRC, MONUSCO kinafuatilia hali ilivyo na kwamba askari wa kikundi hicho wanaolinda amani wamedhibiti uwanja wa ndege wa Goma huku wakifanya doria.

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameshutumu vitendo vya waasi hao na kusema ni kinyume na haki za binadamu za kimataifa na kwamba watawajibishwa kwa vitendo vyao.

Kikundi cha M23 kinajumuisha askari walioasi mwezi Aprili mwaka huu kutoka jeshi la DRC.

Katika hatua nyingine watumishi wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP walioko Goma, wamesema kutwa nzima  ya leo wamelazimika kusitisha usambazaji wa chakula mjini humo kutokana na milio ya risasi inayosikika hapa na pale.

Wolfram Herfuth kutoka WFP amekaririwa akisema kuwa wataendelea kugawa msaada pindi watakapoweza ili kusaidia watu wanaokimbia mashambulizi hayo.