Baraza la Usalama la UM lapitisha azimio kushutumu vitendo vya M23 kuingia Goma, DRC

Baraza la Usalama la UM lapitisha azimio kushutumu vitendo vya M23 kuingia Goma, DRC

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio linaloshutumu vikali kitendo cha waasi wa kikundi cha M23 kuingia na kusonga ndani ya mji wa Goma huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kutishia usalama wa raia.

Azimio hilo limepitishwa kwa kauli moja jumanne usiku na wajumbe wote 15 wa Baraza hilo la baada ya mashauriano yao ya saa kadhaa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Ufaransa ndiyo iliyoandaa rasimu ya azimio hilo ambapo Balozi wake katika Umoja wa Mataifa Gerard Araud amewaambia waandishi wa habari kuwa azimio hilo linataka waasi wa M23 waondoke mara moja huko Goma na kamati ya vikwazo ya Umoja wa Mataifa iangalie uwezekano wa kuwawekea vikwazo makamanda wa waasi hao.

(SAUTI YA GERARD ARAUD)

Wawakilishi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo walishiriki pia mkutano huo wa Baraza la usalama ambapo wameomba Umoja wa Mataifa kuratibu mashauriano ya kuleta amani kwa pande husika katika mgogoro huo kwenye eneo hilo.