Ugonjwa wa Kisukari ni tishio kwa malengo ya maendeleo ya Milenia, tushirikiane kuutokomeza: Ban

14 Novemba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika ujumbe wake wa siku ya kupambana na ugonjwa wa Kisukari hii leo amesema ugonjwa huo ni changamoto kwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea na unazidi kusambaa kila mwaka kutokana na ongezeko la mifumo ya maisha isiyo ya kiafya pamoja na uzee.

Amesema familia maskini zenye mgonjwa wa Kisukari huzidi kutumbukia katika lindi la umaskini na hata mifumo ya kitaifa ya huduma za afya hutindikiwa na kutishia maendeleo ya nchi na kuhatarisha kufikia malengo ya milenia ya mwaka 2015.

Kwa mantiki hiyo Bwana Ban ametaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ziweke mipango ya kinga ya ugonjwa huo ikiwemo utoaji wa huduma za afya ya msingi kwa ajili ya kupima na kutibu ugonjwa huo na kampuni za madawa zitoe dawa na vifaa tiba nafuu vya kupima kiwango cha sukari mwilini.