Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brahimi alihutubia Baraza la Usalama kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano Syria

Brahimi alihutubia Baraza la Usalama kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano Syria

Mwakilishi wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu kuhusu Syria, Lakhdar Brahimi, amelihutubia Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa leo kuhusu juhudi zake za kutafuta amani nchini Syria.

Akizungumza mjini Cairo, Misri mapema leo, Bwana Brahimi amesema anatarajia tangazo kutoka kwa serikali ya Syria kuhusu pendekezo lake la kusitisha mapigano wakati wa wiki hili la Siku Kuu ya Eid Al Adha. Amesema wengi katika upinzani pia wameitikia wito huo kwa njia inayotia moyo.

Kwa upande wao, wanachama wa Baraza la Usalama wamekubali kuwa usitishaji mapigano wakati wa Eid Al Adha unaweza kuwa hatua ya kwanza ya kukomesha ghasia zote kwa njia endelevu, kwa mujibu wa maazimio namba 2042 (2012) na 2043 (2012), na kusisitiza umuhimu wa kuzindua serikali ya mpito, ambayo itaanzisha mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia, na ambao unaenda sambamba na matakwa ya watu wa Syria ya demokrasia, usawa na haki bila kujali asili, kabila au imani zao.