Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi mpya kwa wakimbizi kutoka Somalia kubuniwa Ethiopia

Kambi mpya kwa wakimbizi kutoka Somalia kubuniwa Ethiopia

Idadi ya wakimbizi kutoka Somalia wanaoishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Dollo Ado kusini mashariki mwa Ethiopiam imepita wakimbizi 170,000 kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR. UNHCR inasema kuwa kambi ya Dollo Ado ndiyo ya pili zaidi kwa ukubwa duniani baada ya kambi ya Daadab nchini Kenya ambayo ni makao kwa zaidi ya wakimbizi 400,000 kutoka Somalia.

Andrej Mahecic kutoka UNHCR anasema kuwa serikali ya Ethiopia imeamrisha kufunguliwa kwa kambi ya sita ndani mwa kambi ya Dollo Ado ambayo inatarajiwa kugharamu zaidi ya dola milioni tano kufunguliwa.

Tunatafuta msaada kutoka kwa wafadhili ukiwemo kutoka kwa mashirika yasiyokuwa ya serikali yanayohudumu kambini. Kwenye awamu ya kwanza tunahitaji kwa dharura dola milioni 1.5 kwa maandalizi ya eneo na katika kuweka miundo mbinu kadha na pia katika kuchimba visima, kuweka vituo vya maji, zahati za dharura, choo na kadhalika. Hata kama idadi ya wakimbizi wanaowasili Dollo Ado imepungua mwaka huu, watu wanazidi kukimbia mizozo na kuzorota kwa usalama kusini na kati kati mwa Somalia. Wengi wanasema wanahofu ya kuhangaishwa au kuingizwa jeshini kwa lazima na makundi yaliyojihami yanayodhibiti maeneo makubwa ya nchi.