Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna ushahidi hadi sasa kuwa kirusi kipya cha uambukizi wa njia ya hewa kinaambukizwa miongoni mwa binadamu: WHO

Hakuna ushahidi hadi sasa kuwa kirusi kipya cha uambukizi wa njia ya hewa kinaambukizwa miongoni mwa binadamu: WHO

Shirika la afya duniani, WHO, limesema kuwa hadi sasa hakuna ushahidi kuwa kirusi kipya kinachosababisha uambukizo mkali kwenye njia ya hewa na kushindwa kufanya kazi kwa figo kinaweza kuambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine.

Kauli hiyo ya WHO inakuja baada ya hapo mwezi uliopita mgojwa wa pili kubainika kuwa na kirusi hicho kiitwacho Novel Coronavirus na kusababisha shirika hilo kutoa tahadhari duniani.

Taarifa ya WHO imesema kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa mwingine aliyeripotiwa tangu yule wa pili wa tarehe 22 mwezi uliopita aliyekutwa na kirusi hicho baada ya kutembelea Saudi Arabia ambako pia alipatikana mgonjwa wa kwanza.

Kwa sasa, taarifa hiyo imesema kuwa WHO inazisaidia serikali za Saudi Arabia, Qatar na Uingereza ambazo zinaendelea kushirikiana kupata uelewa mzuri zaidi wa ugonjwa huo na chanzo cha kupata uambukizi.

WHO pia imewataka wahudumu wote wa afya duniani kutoa taarifa za wagonjwa wenye uambukizo mkali katika njia ya hewa.