Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi huko Kadugli, yalazimu UM kuhamisha wafanyakazi wake

Mashambulizi huko Kadugli, yalazimu UM kuhamisha wafanyakazi wake

Umoja wa Mataifa umelazimika kuhamisha wafanyakazi wake kutoka jimbo la Kordofani Kusini nchini Sudan kufuatia mashambulizi ya hapa na pale kwenye mji wa Kadugli jimboni humo ambayo yanakwamisha juhudi za wafanyakazi hao za kutoa misaada kwa wanaohitaji.

Wafanyakazi hao wamehamishiwa katika kituo cha kikosi cha muda cha Umoja wa Mataifa kwa ulinzi wa Abyei, UNIFSA kilichoko eneo linalogombewa na Sudan na Sudan Kusini.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya misaada ya kibinadamu, OCHA imetoa mfano wa makombora ya jana ambayo yalitua katika ofisi za UNICEFU, shule moja kwenye eneo hilo na kituo cha polisi ambapo hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulio hilo.

Msemaji wa OCHA, Jens Laerke amesema kutokana na mashambulizi, Umoja wa Mataifa na washirika wake katika utoaji wa misaada ya kibinadamu yameshindwa kutoa misaada kwa watu walio kwenye eneo la kaskazini mwa jimbo la Kordofan Kusini ambalo linashikiliwa na kikundi cha SPLM.