Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utashi wa kisiasa wahitajika kusaidia wakimbizi:UNHCR

Utashi wa kisiasa wahitajika kusaidia wakimbizi:UNHCR

Ongezeko la hivi karibuni la wakimbizi huko Afrika na Mashariki ya Kati kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo migogoro ya kisiasa limesababisha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kuyataka mataifa ulimwenguni kuwa na utashi wa kisiasa zaidi kuhudumia watu hao wenye mahitaji.

Afisa mwandamizi wa UNHCR Erika Feller akizungumza katika kikao cha mwaka cha kamati ya utendaji ya shirika hilo mjini Geneva , Uswisi, amesema mataifa yanapaswa kujitolea zaidi kusaidia wakimbizi akisema hakuna msaada wa uhakika kutokana na uhaba wa fedha na tabia ya baadhi ya nchi kuona haziguswi moja kwa moja na tatizo la wakimbizi.

Amesema hali hiyo husababisha huduma duni kwa wakimbizi katika kipindi hiki kinachoshuhudia idadi ya wakimbizi ikiongezeka kutokana na migogoro nchini Syria , Sudan , Sudan Kusini , Mali na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo .

Afisa huyo mwandamizi wa UNHCR amesema huduma duni kwa wakimbizi inakwamisha mikakati ya kuzuia watoto kutumikishwa, kuandikishwa kwenye majeshi na kushiriki katika vitendo vya ngono.

Kamati ya Utendaji ya UNHCR hukutana mara moja kwa mwaka kutathmini na kupitisha mipango na bajeti ya shirika hilo pamoja na kutoa ushauri juu ya masuala yanayolihusu na washirika wake.