Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Liberia yakaribia kuandikisha ufanisi wa kusadikika:UM

Liberia yakaribia kuandikisha ufanisi wa kusadikika:UM

Taifa la Liberia limepiga hatua kubwa tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe na ujumbe wa Umoja wa Mataifa sasa ni lazima uanze kupongeza ufanisi huo, na kupunguza msaada wake nchini humo, amesema Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia, UNMIL, Karin Landgren.

Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Bi Landgren amesema, hata hivyo taifa hilo bado lina changamoto kadhaa, na mchango wa Umoja wa Mataifa bado utahitajika kwa serikali ya Liberia, hasa katika kurekebisha sekta ya usalama, maridhiano ya kitaifa, udhibiti wa mipaka, na katika Nyanja zingine ili kuhakikisha kuna amani ya kudumu.

Amesema tangu mwaka 2003, Liberia imejikwamua kutoka taifa lililosambaratika, na kuwa taifa ambalo sasa lipo kwenye mkondo wa demokrasia na amani ya kudumu. Amesema UNMIL sasa inaweza kuanza kuondoka kwa sababu ya mafanikio mengi Liberia, yakiwemo, hatua kubwa katika kuunda tena taasisi za serikali, kujikwamua kiuchumi na kuendeleza harakati za demokrasia.