Uamuzi wa mahakama ya Israel kuhusu kesi ya Rachel Corrie haukuonyesha haki na uajibikaji:UM

30 Agosti 2012

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika maeneo ya Wapalestina yalokaliwa, Richard Falk, amelaani uamuzi ulofanywa wiki hii na jaji mmoja wa Israel wa kuzuia kesi ilowasilishwa na familia ya mwanaharakati wa Kimarekani aliyeuawa na tingatinga Gaza, mwaka 2003

Katika taarifa yake, Bwana Falk amesema uamuzi wa jaji huyo kuwa kifo cha Rachel Corrie kilikuwa ajali ya kusikitisha na kumlaumu mwanaharakati huyo kwa kutoitikia onyo ilotolewa, unaonyesha kushindwa kwa haki na uajibikaji, na ushindi kwa vitendo visivyoadhibiwa vya jeshi la Israel.

Mwanaharakati huyo Rachel Corrie alikuwa anafanya maandamano ya kupinga kubomolewa kwa nyumba ya familia ya Nasrallah, mjini Rafah, ambapo alikuwa akifanya kazi ya kujitolea. Jaji aliamua kuwa hakukuwa na sababu yoyote ya kuifanya serikali ya Israel ilipe fidia, na hivyo kuwaondolea lawama wanajeshi na viongozi wa kisiasa. Bwana Falk amesema kuwa uamuzi huo unakiuka kanuni za mkataba wa Geneva unaoitaka kila nchi inayolikalia eneo la kuzozania kuwalinda raia wakati wote, na hata wahudumu wa kibinadamu.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter