Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban kuhudhuria mkutano wa nchi zisizofungamana na upande wowote nchini Iran

Ban kuhudhuria mkutano wa nchi zisizofungamana na upande wowote nchini Iran

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon atazuru Iran mwishoni mwa mwezi kushiriki katika mkutano wa 16 wa nchi zisizofungamana na upande wowote yaani NAM amesema msemaji wake.

Ameongeza kuwa Ban anauona mkutano huo kama fursa nzuri ya kushirikiana na waku wa nchi na serikali wanaoshiriki mkutano huo ikiwemo mwenyeji wa mkutano katika kupata suluhu ya masuala ambayo ni kitovu cha ajenda za dunia kama kufuatilia matokeo ya mkutano wa maendeleo endelevu wa Rio+20, upokonyaji silaha, kuzuia migogoro, na kuzisaidia nchi zilizo katika kipindi cha mpito.

Mkutano huo utakaofanyika Agosti 26 hadi 31 mjini Tehran chini wa uwenyekiti wa Iran unatarajiwa kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 120 wanachama na pia wawakilishi kadhaa kutoka nchi watazamaji.

Siku za karibuni kumekuwa na taarifa za wito kutoka Israel na Marekani ukimtaka Ban Ki-moon kugomea mkutano huo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Ban Katibu Mkuu anachukulia kwa uzito mkubwa jukumu lake na la Umoja wa Mataifa la kushiriki masuala ya kidiplomasia na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kushughulikia masuala muhimu ya amani na salama.