Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano Wahitajika ili Kuondoa Tishio la LRA:UNOCA

Ushirikiano Wahitajika ili Kuondoa Tishio la LRA:UNOCA

Mwakilishi maalum na mkuu wa afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika ya Kati na maeneo yaloathiriwa na waasi wa LRA (UNOCA), Abou Moussa, ametoa wito kwa Baraza la Usalama na jamii ya kimataifa kuunga mkono utekelezaji wa mkakati wa kikanda wa Umoja wa Mataifa, na mchakato wa ushirikiano wa Muungano wa Afrika, ili kukomesha mateso wanayopitia watu Afrika ya Kati kutokana na vitendo vya waasi wa LRA.

Bwana Abou Moussa amesema, ingawa kamanda mmoja wa LRA amekamatwa hivi karibuni, kundi hilo la waasi bado lina uwezo wa kutekeleza ukatili zaidi kwa watu. Amesema pia ni lazima kuhakikisha kwamba uchunguzi umefanywa kuhusu nani anayelifadhili kundi la LRA. Joshua Mmali, na taarifa zaidi.

Kwa zaidi ya miongo miwili, kundi la LRA limelemaza na kuwaua watu, pamoja na kuwateka nyara wanawake na watoto, na kuwalazimu zaidi ya watu 445, 000 kuhama makwao. Mnamo mwezi Novemba mwaka 2011, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliiomba afisi ya UNOCA kushirikiana na Afisi ya Umoja wa Mataifa kwenye Muungano wa Afrika, ili kuweka mikakati ya kukabiliana na suala la LRA.

Mkakati uliowekwa unahusu kuwalinda raia, kupanua shughuli za usalimishaji silaha na urejeshwaji wa waasi katika jamii, kusaidia mipango ya utoaji huduma za kibinadam na kuwalinda watoto, pamoka na kuzisaidia serikali katika maeneo yaloathiriwa katika masuala ya amani, haki za binadam, uongozi wa kisheria na maendeleo.