Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Washukiwa wa kivita Sudan wakamatwe:Ocampo

Washukiwa wa kivita Sudan wakamatwe:Ocampo

Mwendesha mashtaka mkuu kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC Luis Moreno Ocampo amelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataiafa kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa viongozi wanaotuhumiwa kuhusika kwenye uhalifu wa kivita nchini Sudan wamekamatwa.

Akihutubia mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Ocampo amesema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni kukamatwa kwa watu hao akiongeza kuwa ni jukumu la baraza hilo kuhakikisha serikali ya Sudan imetoa ushirikiano.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliomba mahakama ya ICC iliyo na makao yake mjini Hague nchini uholanzi kuchunguza uhalifu wa kivita kwenye jimbo la Darfur mwaka 2005 baada ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kubaini kuwa kulifanyika vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.